Serikali ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza ikiwa nchi inakabiliwa na janga la njaa na wala si taasisi, asasi za kiraia au wanasiasa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo, alipokuwa akitoa maoni yake kuhusu mijadala mbalimbali inayoendelea katika vyombo vya habari kwamba Tanzania inakabiliwa na tatizo la njaa.
Cheyo amesema kuwa, huwezi kusema nchi ina njaa wakati vyakula vipo katika masoko mbalimbali hapa nchini.
Amewataka watanzania kutofautisha kupanda kwa bei za vyakula na janga la njaa.
Aidha, Cheyo amesema kuwa tatizo hilo tayari limetatuliwa na Serikali kwa kutoa tani milioni 1.5 za mahindiĀ ambazo zitasambazwa nchi nzima kwa ajili ya wananchi kununua.
Hata hivyo, Cheyo amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa mahindi hayo kuuzwa kwa uangalifu kwani gharama yake itakuwa ni ya chini, hivyo kuna watu ambao watajitokeza kununua kiasi kikubwa na kwenda kuhifadhi kwa ajili ya kuuza kwa gharama ya juu baadae.
Vile vile amewataka watanzania kuwa na tabia ya kutunza vyakula badala ya kuuza vyakula vyote mara wanapovuna, ili vyakula hivyo viweze kuwasaidia pale ambapo mvua zinakuwa zimechelewa kama ambavyo imekuwa kwa mwaka huu.