Mshambuliaji kutoka DR Congo na klabu ya Young Africans Chico Ushindi Wa kubanza amewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, baada ya kushindwa kucheza michezo kadhaa tangu aliposajiliwa Januari 2022.
Chico alisajiliwa Young Africans wakati wa Dirisha Dogo la Usajili akitokea TP Mazembe ya nchini kwao DR Congo, na alitarajiwa kuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha klabu hiyo ambacho msimu huu kimedhamiria kurejesha heshima ya kuwa Mabingwa wa Tanzania Bara.
Mshambuliaji huyo amesema Viongozi wamekua wakimueleza namna Mashabiki wanavyochukizwa na hali yake ya kushindwa kucheza, jambo ambalo amekiri linamuumiza.
Amesema Majeraha na kuugua Malaria ndio sababu kubwa ya kushindwa kuwajibika ipasavyo kama alivyotarajiwa, lakini amewasihi kuendelea kumuamini na muda utakapofika atawafurtahisha.
“Viongozi wameniambia kwamba watu wanaumia mimi kuona sichezi, ni hii malaria imenivurugia, lakini yatapita. Mashabiki wasubiri kuniona mchezo unaokuja watafurahia kazi yangu hapa,” amesema Chiko
Usajili wa Chiko ulitumika kwenye dili la kuuzwa kwa Kiungo Mukoko Tonombe aliyetimikia TP Mazembe akitokea Young Africans mwezi Januari 2022.