Rapa Chid Benz ambaye hivi karibuni amerejea rasmi kwa nguvu kwenye muziki baada ya kupotea kwa muda kutokana na athari za matumizi ya dawa za kulevya, amesema hatazisahau fadhira na upendo wa dhati wa Mr Blue.

Akifunguka katika  kipindi cha The Playlist cha 100.5 Times Fm Jumamosi iliyopita, Chid alisema kuwa ingawa ana wadogo zake wengi kwenye muziki wanaompenda, Mr Blue ndiye mdogo wake namba moja aliyekuwa naye siku zote akimsaidia na kumshauri kwa moyo hadi akawa anatoa machozi.

“Ni kweli katika watu wote katika hii dunia, ambaye hakuniacha kabisa ni yeye [Mr. Blue],” alisema Chid Benz.

Mr Blue

Rapa huyo alisema kuwa Mr Blue hakuchoka kumpa ushauri hata kwa muda wa saa mbili hadi tatu mfululizo na kwamba alipokuwa akiona kama hajaeleweka vizuri aliendelea kusisitiza hadi akatokwa na machozi.

King Kong, kama anavyopenda kujiita alieleza pia kuwa anaikumbuka siku ambayo alimuona Mr Blue akiwa mwenye huzuni kubwa maeneo ya maskani yake na alipozungumza naye alionesha kusikitishwa na hali ya rapa huyo na akampa sharti moja ili afute machozi yake.

“Nikamwambia mbona uko hivyo? Akanambia ‘daah umepungua sana… unajua hilo?’ Nikambia eeh mbona mimi naona kawaida tu. Akaniambia ‘basi jua umepungusa sana, ukitaka mdogowako nisiwe naumia na nalialia hovyo, jaribu kuwa sawa’. Nikamwambia haina noma, nikajikata,” alisema.

Chid alisema kuwa anamuamini sana Mr Blue kwenye muziki na kwamba hata alipokuwa kimya alihisi bado yupo kwenye game akiwakilishwa vizuri na mdogo wake huyo.

Chid Benz amerudi kwa kishindo kwenye muziki na ngoma yake mpya ya ‘Chuma’ aliyomshirikisha Raymond wa WCB. Hivi sasa rapa huyo anasaidiwa na meneja wa Diamond na Tip Top, Babu Tale.

 

Azam FC Yahamishia Kambi Visiwani Zanzibar
Picha: Matukio 4 ya Mwisho wa Wiki