Chifu wa kabila la wagogo, Henel Mazengo wa pili, amemtupia lawama Ofisa Mtendaji wa kata ya Mvumi Makulu, Chamwino jijini Dodoma kwa kukata mti wa kimila.
Chifu Mazengo ameeleza kitendo cha kukatwa kwa mti huo kimemuondolea mizimu yake aliyokuwa anatumia kwenye kazi zake na kumtaka ofisa huyo kurudisha mizimu hiyo.
“Mimi ninachotaka ni watu wangu (mizimu) warudi kwa sababu hapa nilipo siwezi kufanya shughuli zozote za kichifu kwa sababu watu wangu hawapo” amesema Chifu huyo.
Amebainisha kuwa yeye ameshindwa kurejesha mizimu hiyo ambayo ni nyuki wa kizimu kwa sababu imekataa kurudi kwani nyumba yao imeharibiwa.
Ofisa huyo amejitetea kwa kusema alikuwa hajui kama mti huo ilikuwa unatumiwa kwa shughuli za kimila na ndiyomaana alitoa kibali cha mwananchi kukata mti huo kwaajili ya shughuli zake za ujenzi.
Aidha ameongeza kuwa yeye pia hawezi kuwarudisha nyuki hao hivyo ameomba waende kwenye vyombo vya sheria kwani tokea ameanza kazi hapo, hajawahi kuambiwa kuwa ule mti ni wakimila na mwenye jukumu la kusema ni chifu mwenyewe ambaye hakufanya hivyo.