Nchi ya Chile imeteuliwa kuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali wa michuano ya klabu bingwa Amerika ya kusini (Copa Libertadores) kwa mwaka 2019.
Shirikisho la soka barani humo (CONMEBOL) limetoa taarifa ya kuthibitisha mchezo huo kuchezwa nchini Chile katika uwanja wa taifa mjini Santiago mwezi Novemba.
Shirikisho hilo pia limeuteuwa uwanja wa taifa wa Peruuliopo uliopo mjini Lima nchini Peru, kuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali wa michuano ya kombe la shirikisho (Copa Sudamericana) mwaka 2019.
Maamuzi hayo yamefikiwa baada ya mkutano mkuu wa CONMEBOL uliofanyika jana Jumanne, huku ikiaminika viwanja hivyo vinakidhi vigezo vya kuwa mwenyeji wa michezo hiyo mikubwa upande wa klabu kwenye bara la Amerika ya kusini.
Wakati huo huo CONMEBOL wamefanya mabadiliko ya kanuni za mchezo wa fainali, ambapo sasa utachezwa katika uwanja huru, tofauti na ilivyo sasa ambapo timu husika hucheza michezo ya nyumbani na ugenini.
Kanuni hiyo pia itaziwezesha klabu husika kupata asilimia 25 ya mapato ya milangoni.