Mvutano wa kibiashara waendelea kati ya Marekani na China huku nchi hizo zikitoa kauli zinazokinzana wakati ambapo Rais Trump ameamua kuongeza ushuru maradufu kwa bishaa za China.
China na Marekani zimetoa taarifa zinazotofautiana juu ya mazungumzo ya biashara, ambapo China imesema kuwa bado ina matumaini kuhusu kuutatua mvutano wa kibiashara, wakati Marekani imesema imeongeza ushuru mara mbili kwa bidhaa kutoka China.
Mjumbe wa China katika mazungumzo na Marekani, Liu He ameonya kwamba kuna viwango ambavyo nchi yake haitakuwa tayari kuvivuka.
Makamu wa waziri mkuu wa China Liu He amesema kuwa mazungumzo kati ya nchi yake na Marekani hayajavunjika licha ya kuwepo vikwazo vidogo ambavyo ni vya kawaida na kwamba China itaendelea kuwa na mtazamo chanya juu ya mazungumzo ya biashara na Marekani licha ya Rais Trump kuamua kuziongezea ushuru bidhaa za China.
Maoni ya Liu yanakinzana na ya waziri wa fedha wa Marekani,Steve Mnuchin ambaye aliwaambia waandishi wa habari wa CNBC kwamba hakuna mazungumzo yoyote ya biashara yaliyopangwa kufanyika kati ya nchi hizo mbili kwa sasa.
Aidha, Rais wa Marekani, Donald Trump amejisifu kwa kuandika kwenye Twitter kwamba ameikomoa China kwa kiasi ambacho labda nchi hiyo haitotaka kurudi kwenye meza ya majadiliano kabla ya uchaguzi wa 2020.
Marekani imechochea vita vya biashara kwa kuongeza ushuru kwa thamani ya dola bilioni 200 kwa bidhaa za China zinazoingia nchini humo ambapo wachambuzi wa China wamesema kuwa huenda Marekani haina utayarifu kwa kile inachoweza kuhimili.
Hata hivyo, siku ya Ijumaa, Rais Donald Trump aliweka vikwazo vipya dhidi ya bidhaa zinazoingia Marekani kutoka China, hatua hiyo iliongeza ushuru kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 kwenye bidhaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na simu za mkononi, kompyuta na vitu vya kuchezea watoto.