Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Liu Jieyi amesema kwamba suluhu ya nguvu za kijeshi inayotaka kufanywa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini haifai kupewa kipaumbele.
Liu Jieyi amesema hayo katika kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa akijibu hatua ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio kombora lake la masafa marefu.
Hayo yamejiri baada ya Marekani kutangaza kuwa itatumia nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini ‘iwapo ni lazima’ kufuatia jaribio la kombora la masafa marefu lilotekelezwa na taifa hilo.
Liu Jieyi alirejelea wito wa China na Urusi kwa mazungumzo ya Korea Kaskazini kusitisha majaribio ya makombora iwapo Marekani na Korea Kusini zitasitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi.
Awali balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa Nikki Haley alisema kuwa vikwazo vya kimataifa vilivyowekewa Pyongyang kwa miaka kadhaa havitoshi.
Amesema kuwa vitendo vya Korea Kaskazini ni ishara za kuzuka kwa mgogoro duniani.