Balozi wa Marekani ameitwa na wizara ya mambo ya kigeni ya China kwa madai ya kutaka Marekani iondoe sheria iliyopitishwa bungeni ikiunga mkono vuguvugu la maandamano ya kudai demokrasia mjini Hong Kong, vinginevyo italazimika kupambana na hatua kali.
Mswada wa Hong Kong unaosubiri kutiwa saini na rais Donald Trump unaunga mkono haki za binadamu na demokrasia katika mji huo, wakati ukitishia kuondoa hadhi maalumu ya eneo hilo ya kiuchumi.
Pia unapiga marufuku uuzaji wa mabomu ya kutoa machozi, risasi za mipira na vifaa vingine vinavyotumiwa na majeshi ya usalama kukandamiza maandamano ya kudai demokrasia.
Wizara hiyo imesema Naibu waziri Zheng Zeguang amemwita balozi wa Marekani Terry Branstad jana Jumatatu kuelezea upinzani mkali kuhusiana na mswada huo.
Trump hajaonesha ishara iwapo atatia saini mswada huo kuwa sheria, kwani wiki iliyopita alisema kuwa wakati akiwaunga mkono watu wa Hong Kong , pia anamuunga mkono rafiki yake rais wa China Xi Jinping.