Klabu ya Kagera Sugar imeendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao na tayari imetambulisha wachezaji sita wapya akiwemo Mzambia Obrey Chirwa anayetarajiwa kuongeza uzoefu katika safu ya ushambuliaji.
Timu hiyo yenye masikani yake mkoani Kagera tayari imewanasa Richardson Ng’ondya kutoka Mbeya City, Cleophace Mkandala aliyekuwa Azam FC, Ally Ng’anzi kutoka Loudo United ya Marekani, Dickson Gidion kutoka Atlabara ya Sudan, Abuiudy Mtambuka kutoka Mashujaa na Chirwa aliyekuwa Ihefu FC wote wakipewa mikataba ya miaka miwili.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Mecky Mexime amesema wanazingatia ubora na uzoefu kwa wachezaji wanaowasajili hivyo ongezeko la Chirwa litasaidia sana hususan eneo la Ushambuliaji.
“Tunafanya usajili kulingana na matakwa ya timu. Kama unavyojua, ligi kila mwaka ushindani unaendelea kuongezeka, hivyo lazima uwe na wachezaji wa kutosha wenye ubora na uzoefu. Mfano kama Chirwa ni mzoefu na ligi na ana nguvu hivyo kama atatusaidia katika eneo la ushambuliaji kutokana na uzoefu wake.” amesema Mexime aliyesisitiza bado chama lake halijamaliza kutangaza wachezaji wapya.
Kabla ya Kagera Sugar Chirwa alitamba na Klabu za Young Africans na Azam FC.