Uongozi wa Simba SC rasmi umetangaza kuachana na Kocha wa Walinda Lango kutoka nchini Morocco Chlouha Zakaria.
Simba SC imetangaza maamuzi hayo leo Alhamis (Juni 15) kupitia vyanzo vya habari vya klabu hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuboresha Benchi la Ufundi kuelekea msimu ujao 2023/24.
Kocha Zakaria alijiunga na Simba SC Novemba mwaka jana (2021), na alibahatika kufanya kazi na Kocha Mgunda kabla ya kuwasili kwa Kocha Mkuu Robertinho mwanzoni mwa mwaka huu akitokea Vipers SC.
Taarifa ya kuondoka kwa Kocha huyo imeeleza: “Kutokana na maboresho makubwa ya timu ambayo tumejipanga kufanya tumekubaliana kutoendelea na Kocha Chlouha Zakaria.
Simba SC inamshukuru Zakaria kwa kazi kubwa aliyofanya akiwa na kikosi chetu na tunamtakia kila kheri katika maisha yake mapya ya mpira huko aendako.
Uongozi wa Klabu unaendelea na mchakato wa kutafuta mbadala wa Zakaria kabla ya kuanza kwa maandalizi ya msimu mpya (Pre-Season).