Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Daniel Chongolo ‘amemshtukia’ Mkandarasi anayejenga Barabara ya Kibaoni – Stalike, kwa kiwango cha lami, baada ya kukagua na kushuhudia ujenzi wa barabara hiyo ukisuasua na kuwa nyuma ya muda, kinyume cha mkataba.
Kufuatia hali ya kusuasua kwa ujenzi wa barabara hiyo muhimu inayotarajiwa kuufungua zaidi Mkoa wa Katavi kuunganisha na mikoa jirani ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga kukutana na uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania – TANROADS, Mshauri Mwelekezi na Mkandarasi CSRG, ili kuhakikisha kasi ya ujenzi inaongezeka kulingana na mkataba.
Maelekezo hayo, yametolewa baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo iliyopo Wilayani Mlele Katavi Oktoba 4, 2023 wakati akiendelea na ziara yake ya kuimarisha uhai wa chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 na kusikiliza changamoto za wananchi.
Amesema, “wakati wa kuhitimisha ziara yangu Oktoba 7, 2023, atakuja Waziri wa Ujenzi. Nimemuita tukutane Mpanda hapo, aje mwenyewe kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kuwaeleza wananchi ni namna gani barabara hiyo itakamilishwa kwa kasi inayotakiwa,” amesema Komredi Chongolo.
Barabara hiyo (Km 50) itakayogharimu zaidi sh. Bil. 80, inajengwa na Kampuni ya China ya CRSG. Ujenzi wa barabara ulianza Juni 23, 2022 na unatarajiwa kukamilika Juni 22, 2025 ambapo Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi, Albert Laizer amesema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 11.2 nyuma ya utekelezaji ambao ulipaswa uwe asilimia 21.