Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi -CCM, Daniel Chongolo amezungumza na Wanachama wa CCM pamoja na Wananchi aliposhiriki Mkutano wa Shina Namba 9, Tawi la Kalakala, kwa Balozi, Salvatory Damian wa Kata ya Muze, Jimbo la Kwela Sumbawanga Vijijini, wakati wa ziara yake ya kuimarisha uhai wa Chama, kusikiliza kero na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama ya 2020-2025, Mkoani Rukwa.
Akiwa katika tawi hilo, Chongolo ameahidi kuishinikiza Serikali kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Muze ambacho kitahudumia wananchi wengine wa maeneo ya karibu pia, na kuhakikisha ujenzi wa barabara inayopita Mlima Lyamba lya Mfipa, hasa kuanzia eneo la Kizungu hadi Muze – Kata ya Muze, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (Km 12), unaharakishwa.
Aliwaambia kuwa kipande hicho nacho kinatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka, kama ambavyo tayari kipande cha kutokea Ntendo hadi Kizungu, chenye urefu wa kilometa 25, kinaendelea kujengwa na mkandarasi yuko eneo la mradi, ili hatimae kero ya usafiri, usafirishaji na uchukuzi wa abiria na mizigo mtawalia, kutoka maeneo hayo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao, inafika mwisho.