Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Ndugu Daniel Chongolo amekagua Skimu ya Umwagiliaji ya Ugalla katika Kijiji cha Katambike Wilayani Mpanda, ili kuuwekea mpango wa kuukwamua, baada ya mradi huo kukwama tangu 2007.
Chongolo amefanya ukaguzi wa skimu hiyo iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 800 wakati wa ziara ya kuimarisha uhai wa chama ya hii leo Oktoba 6, 2023, kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 katika Halmashauri ya Nsimbo, Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi.
Akizungumza na Wananchi wa maeneo ambao ndiyo walikuwa walengwa na wanufaikaji wa Skimu ya Umwagiliaji hiyo inayotegemea maji ya Mto Ugalla, amesisitiza kuwa mradi huo unapaswa kufanya kazi ili wakulima wa maeneo hayo waendelee kufanya kilimo na kuzalisha zaidi.
“Mradi huu wa skimu ya umwagiliaji umekwama tangu mwaka 2007. Zinatajwa tu fedha hapa, ziliingia zikaingia, lakini watu wanawashangaa kuwa hizo fedha zilienda wapi? Nitakwenda kuzungumza na Waziri mwenye dhamana na Kilimo ili aone namna ya kuukwamua mradi huu ambao tija yake ni kubwa endapo utafanya kazi,
Akiwa katika eneo hilo, Chongolo pia amesisitiza kuwa mradi huo inatakiwa ufanyike usanifu wa kina unaoendana na mazingira husika, ili upatikane mradi ambao utakua endelevu na wa uhakika.