Mabingwa wa soka Barani Ulaya FC Bayern Munich wamekamilisha dili la usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Cameroon Jean-Eric Maxim Choupo-Moting, kwa uhamisho huru.
Msimu uliopita Choupo-Moting aliwatumikia mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain, ambao walimsajili mwaka 2018 akitoke Stoke City ya England.
Hata hivyo hii itakua si mara ya kwanza kwa mshambuliaji huyo mwenyeumri wa miaka 31 kucheza Ligi ya Ujerumani, kwani aliwahi kutumika miaka ya nyuma akiwa na klabu za Hamburg, Nurnburg, Mainz na Schalke.
Baada ya kutua Allianz Arena na kusaini mkataba wa mwaka mmoja Choupo-Moting alizungumza na waandishi wa habari na kusema: “Ni hisia nzuri kurejea katika Bundesliga halafu kwenye klabu kubwa Ujerumani,”
“Ni nani asietaka kuchezea Bayern Munich? Ni heshima kubwa kucheza kwenye hii klabu, lengo ni kushinda kila taji, nina shauku kubwa ya kufanikisha malengo haya.”
Mkurugenzi wa michezo wa FC Bayern Munich Hasan Salihamidzic naye amesema: Nina furaha kufanikisha kumsajili Choupo-Moting, anaongeza uimara wa kikosi chetu, hasa kwenye eneo la kati ambalo tumekuwa tukihitaji kuimarika.
“Eric amepata uzoefu wa kimataifa alipokuwa Paris Saint-Germain, anaijua vyema Bundesliga na anakuja kwa uhamisho huru atatufaa sana.
Usajili wa Choupo-Moting umekamilishwa siku moja baada ya Marc Roca kujiunga na klabu hiyo akitokea Espanyol kwa kitita cha €15m.