Kiungo kutoka nchini Denmark Christian Eriksen anaweza kucheza mchezo wake wa kwanza Manchester United tangu Januari mwaka huu wakati Mashetani Wekundu watakapowakaribisha Everton leo Jumamosi (April 08), kwa mujibu wa Kocha, Erik ten Hag.
Eriksen hajacheza tangu katika mchezo wa ushindi wa Kombe la FA dhidi ya Reading mwishoni mwa Januari, baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu wakati wa mechi hiyo.
Hapo awali United walishughulikia kukosekana kwa kiungo huyo vyema waliponyanyua Kombe la EFL Februari, ingawa vijana hao wa Ten Hag walivumilia msururu wa michezo mitatu bila kushinda katika Ligi Kuu England kabla ya Jumatano kushinda bao 1-0 dhidi ya Brentford.
Alipoulizwa kama Eriksen anaweza kurejea katika kikosi kitakachoikabili Everton baada ya ushindi huo, Ten Hag aliiambia Viaplay ya Denmark: “Tutaona.”
“Anaendelea. Amerejea tu katika mazoezi ya timu wiki hii. Tuna vikao viwili. Baada ya hapo, tutaamua kama atarejea kikosini tena.” United wameshinda asilimia 63.2 ya michezo ya Ligi Kuu England, Eriksen amecheza msimu huu (12 kati ya 19), ikilinganishwa na asilimia 44.4 ya michezo ambayo amekosa (nne kati ya tisa).