Mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara misimu ya 1998/1999 na 1999/2000 Mtibwa Sugar, wamefanikiwa kunasa saini ya wachezaji wawili waliofanya vyema katika timu zao msimu uliopita.
Usajili uliofanywa na klabu ya Mtibwa Sugar ni mikakati ya kuboresha kikosi kuelekea msimu ujao, nyota waliosajiliwa hadi sasa ni mshambuliaji matata kutoka timu ya Polisi Morogoro Salum Ramadhani Kihimbi maarufu “Chuji”.
Nyota mwingine ni Hussein Idd aliyenaswa kutoka katika timu ya jeshi ya JKT Oljoro na anamudu kucheza nafasi ya beki wa kati.
Nyota wote wawili wameingia kandarasi ya kuitumikia Mtibwa Sugar kwa miaka miwili.
Aidha mbali na nyota hao kocha mkuu Zuber Katwila kwa kushirikiana na benchi la ufundi wamesema watapandisha baadhi ya vijana kutoka katika timu ya vijana ya Mtibwa Sugar.
Uongozi wa Mtibwa Sugar unaendelea kufanyia kazi mapendekezo ya benchi la ufundi, hivyo basi usajili bado unaendelea na nyota wengine wanatarajiwa kuingia makubaliano na Mtibwa Sugar.
Pia uongozi wa klabu ya Mtibwa Sugar umewataarifu wapenzi na mashabiki wake kuwa kuna baadhi ya nyota ambao mikataba yao imefikia tamati ambao ni Jaffary Salum Kibaya , Said Mkopi, Maulid Gole “Adebayor”, Said Bahanuzi, Vicent Barnabas, Ally Lundenga na Ally Shomary.