Kiungo wa Singida Fountain Gate, Morice Chukwu amesema changamoto kubwa aliyoikuta katika mechi yake ya kwanza ndani ya timu hiyo mpya licha ya kutoa asist na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita ni umaliziaji.
Morice aliyesajiliwa ndani ya timu hiyo akitokea Rivers United ya Nigeria, alitambulishwa akiwa miongoni mwa wachezaji 17 wapya, ambao wataitumikia Singida Fountain Gate msimu huu.
Chukwu amesema licha ya mchezo kuwa mzuri amegundua kuwa anahitaji mazoezi zaidi katika eneo la kufunga ili kufanya makubwa katika Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.
Chukwu amesema licha ya tatizo hilo, anafurahia kila kitu ndani ya Singida FG, hasa ushirikiano wa wachezaji katika mchezo wa kwanza ambao walicheza kama walishakaa pamoja misimu mitatu mfululizo.
“Nauona msimu ujao ukiwa wa mafanikio makubwa kama tukiendelea hivi, kwani nimekutana na wachezaji wenye morali na shauku ya mafanikio zaidi.” amesema Morice Chukwu
“Kocha alifurahi na kutupogeza kwani kwetu ulikuwa mwanzo mzuri ambao ulitupa mwanga wa aina ya kikosi tulichonacho, lakini kubwa zaidi ni kwa mara ya kwanza kucheza timu mpya na kutoa asisti, kwangu si jambo dogo.
Singida FG itaanza msimu kwa kucheza mashindano ya Ngao ya Jamii kwa mara ya kwanza ikitarajia kukutana na Simba SC, Agosti 10.