Chuo kikuu cha Mtakatifu Agustino kampasi ya Mwanza kinatarajia kuzindua umoja wa wanazuoni (Alumni ) waliowahi kuhitimu chuoni hapo tangu kuanzishwa kwake.
Hayo yamejiri baada ya viongozi wakuu wa chuo hicho kukutana kwa ajili ya kikao cha awali kujadili uanzishwaji wa SAUT Alumni mnamo mwezi April.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Mwenyekiti mteule wa umoja wa wanazuoni hao Pius Lufufu amesema kuwa uzinduzi rasmi wa Alumni ni kwa ajili ya kuwatambua wanazuoni wote waliowahi kuhitimu chuoni hapo pamoja na wao kushiriki katika kuendeleza chuo kupitia miradi mbalimbali.
Aidha, Lufufu amesema chuo pia kitawasaidia Alumni hao kuwatafutia fursa mbalimbali pamoja na kushirikiana nao kwa ukaribu ili kuweza kuchochea maendeleo.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Balozi Profesa Costa Ricky Mahalu ametoa wito kwa wote waliowahi kusoma chuoni hapo kuwa Alumni ni kwaajili ya manufaa ya wote.
“Nina imani kabisa kwamba uzinduzi wa Alumni utawanufaisha wengi ikiwemo pia kuisaidia jamii ya chuo chetu hiki. Hivyo ni wito wangu kwamba wanazuoni wahitimu watakuwa tayari kwa ajili ya kuking’arisha chuo chetu na kukifanya kuwa sehemu endelevu ya kupata elimu bora katika mazingira wezeshi,” amesema Profesa Mahalu.