Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema Chuo Kikuu cha India kinatarajia kumtunuku Shahada ya heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Makamba amesema, Chuo hiko kikuu cha Waharlal Nehru kilichopo jijini Delhi kimefikia uamuzi huo baada ya kutambua mchango wa Rais Samia wa kuunganisha nchi hizo mbili (India na Tanzania).
Amesema, “tumepata taarifa rasmi kuwa Chuo Kikuu kinachoheshimika hapa India cha waharlal Nehru kimeamua kumtunuku Rais wetu Degree ya Heshima, Shughuli hii itafanyika tarehe 10 chuo hiki ni namba moja wamesoma watu muhimu hapa akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje sasa hivi, Waziri wa Fedha na wengine wengi.”
Aidha ameongeza kuwa, “wameamua kufanya hivyo kwa kutambua mchango wake katika diplomasia ya uchumi, mafanikio katika kusukuma maendeleo yanayogusa watu moja kwa moja katika Nchi yetu, mafanikio katika kuimarisha mahusiano ya Kimataifa kwa ujumla kwenye Umoja wa Mataifa.”
“Sisi tunashukuru Mheshimiwa Rais anatambuliwa, anatambulika na anaheshimika hata kwenye Mataifa mengine kwa kazi kubwa anayofanya katika Mataifa mengine,” amesema Waziri Makamba ambaye pia alipata wasaa wa kusalimiana na Wanafunzi wa Kitanzania wanaoendelea na Masomo Nchini India.