Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) limesema kuwa linaamini kwamba Mwanamfalme Mohammed Bin Salman wa Saudi Arabia ndiye aliyeamrisha kuuawa kwa mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa nchi yake Istanbul.
Vyanzo kutoka ndani ya shirika hilo vililiambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba CIA ilishaviarifu vyombo vyingine kwenye serikali ya Marekani, likiwemo baraza la Congress, juu ya ugunduzi wake huo ambao unapingana na msimamo wa serikali ya Saudi Arabia kwamba Mwanamfalme Mohammed hakuhusika na mauaji hayo.
Aidha, tathmini hiyo ya CIA, ambayo kwanza iliripotiwa na gazeti mashuhuri la Washington Post ambalo Khashoggi alikuwa akiliandikia, ni ya hali ya juu kutolewa na Marekani hadi sasa ikimuhusisha na mtawala huyo wa Saudi Arabia moja kwa moja na mauaji hayo.
Hata hivyo, gazeti la Washington Post liliandika kuwa CIA pia ilichunguza simu iliyopigwa kutoka ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul baada ya mauaji ya Khashoggi. Maher Mutreb, afisa usalama ambaye mara kadhaa ameonekana akiwa na Mohammed bin Salman, alimpigia simu Saud al-Qahtani, msaidizi wa ngazi za juu wa Bin Salman, akimfahamisha kuwa operesheni ilikuwa imekamilika.