Mkuu wa Benchi La Ufundi Azam FC, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa anapenda kushinda mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Young Africans.
Mchezo huo unaosubiriwa na mashabiki wengi wa soka nchini, unatarajia kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili hii, ambapo Azam FC imetoka kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbao FC juzi Jumapili.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Cioaba alisema kuwa atafanyia kazi na kurekebisha makosa yote yalijitokeza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbao FC ili kuhakikisha anavuna ushindi.
“Ni mchezo mmoja ambao kuna uwezekazo tukashinda sisi au ikashinda Yanga, lakini napenda Azam FC ishinde mchezo huu ili kuwania nafasi ya juu na kuendelea kukaa juu,” alisema kwa ufupi kocha huyo raia wa Romania mwenye leseni ya juu ya ukocha (UEFA Pro Licence).
Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuingia kambini leo Jumanne, tayari kwa maandalizi ya mchezo huo. Azam FC hivi sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 57, pungufu ya pointi 15 na kinara Simba, iliyojikusanyia 72.