Shahrukh Mohamed Khan ni msanii maarufu wa filamu nchini India. Akiwa kwenye shughuli zake za kuigiza anaweza akakufanya usitamani filamu iishe.

Anaweza akakufanya usitamani hata kula ili tuu uendelee kuiangalia filamu yake, kwa wale ambao wenye hisia kali hudiriki hata kutoa machozi, kwani anasisimua sana katika kazi zake.

Ndiyo, jamaa ni fundi kweli kweli kama hauamini tazama sinema ya “KAL HO NAA HO” kama hiyo ni cha mtoto, jitahidi kuangalia filamu yake iitwayo “KHABI KHUSHI KABHIE GHAM”. Kwenye kazi zake hutendea haki visa na mikasa anavyoviigiza kiasi kwamba huwavutia watazamaji.

Wakati nilipokuwa mdogo nilikuwa napenda kutazama filamu katika vibanda umiza, siku ikiwekwa filamu ya Shahrukh watu walikuwa wakijazana sana.

Iliwahi kutokea siku moja nilikuta watu wakipiga mayowe kana kwamba kulikuwa na mechi ya Simba na Yanga au ya Manchester United dhidi ya Liverpool na tayari lishafungwa bao, la khasha! kumbe haikuwa hivyo bali iliwekwa sinema ya ‘KUCH KUCH HOTA HAI’.

Kwani watu hawa walifurahia filamu hii? hili swali jepesi sana, waliburudika kwa sababu waliitazama kazi nzuri kutoka kwa msanii mwenye kipaji na mvuto.

Tuache kumuongelea Shahrukh pekee tuje kwenye hoja ya msingi ya kumfananisha Chama na huyu gwiji aliyeiteka dunia.

Claotus Chama au ‘MWAMBA WA LUSAKA’ kama anavyopenda kumuita rafiki yangu Baraka Mpenja.

Kipindi aliposajiliwa Simba SC wapo baadhi ya watu walimbeza, licha ya kwamba ofisa habari Haji Manara alitumia nguvu kubwa kuwaaminisha Kuwa wamepata kifaa, lakini wengine hawakuamini. Unajua kwanini? ngoja nikwambie, ni kwa sababu kwa miaka ya nyuma vilabu vya Simba na Yanga vilikuwa vikisajili wachezaji kutoka nje ya nchi ambao uwezo wao ulikuwa mdogo kulinganisha na wazawa.

Mfano Simba ilimleta Pape Ndaw, Danny Serunkuma na wengine wengi mwishoni walichemka tuu.

Lakini kwa huyu Chama mambo yalikuwa tofauti kwani mechi yake ya kwanza tuu aliwasha moto mno. Nakumbuka ilikuwa ni mechi kati ya Simba na Asante Kotoko ya Ghana kwenye tamasha la Simba Day ambalo hufanyika kila inapofika mwezi Agosti.

Itaendelea.

Credit Mvulla Hassan.

KKKT yasitisha ibada dayosisi ya Karagwe
Thierry Henry mchezaji bora England