Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chama amekanusha uvumi unaoendelea kusambaa kuhusu mpango wa kuwa njiani kujiunga na Young Africans, kufuatia mkataba wake na Simba SC kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.
Young Africans wanadai kuwa katika mstari mzuri wa kumsajili kiungo huyo mahiri, kwa kigezo cha kuwa mchezaji huru itakapofika mwishoni mwa msimu huu, lakini Simba SC wamekua wakisisitiza bado mchezaji huyo ana mkataba nao.
Chama amekanusha uvumi huo kwa njia ya Video na kuandia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kwa kueleza kuwa, bado ana mkataba na Simba SC, na anafurahia maisha ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake makuu mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam.
Kiungo huyo aliyefunga mabao muhimu kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu uliopita dhidi ya Nkana FC na AS Vita, ameandika: “Ninachukia taarifa za fununu, acha niliweke hili sawa, klabu nitakayoitumikia katika ligi ya Tanzania ni Simba SC.”
Makamu Mwenyekiti wa Young Afcans Fredrick Mwakalebela jana Jumatatu alieleza mipango ya kumfuatilia nyota huyo ambaye alidai kuwathibitishia kuwa mkataba wake uliobaki ni chini ya miezi sita.
“Mwakalebela alisema wanaamini, Chama amebakiza mkataba wa miezi sita (6) tofauti na klabu ya Simba inavyosema kwamba bado mchezaji huyo anamkataba wa miaka miwili.”
“Wenzetu wameweka dau wamesema wanataka Dola za Marekani 350,000 ili kumpata Chama ingawa tunajua kabisa amemaliza mkataba. Ningependa kusema kwamba, tunafatilia kwa karibu na tumeanza mazungumzo na Chama na ikiwezekana tungependa aweze kuchezea Young Aficans.”
“Kama tutakubaliana vigezo na masharti ambayo ameyatoa yeye basi atakuwa mchezaji wetu. Nisingependa niwahakikishie wapenzi na wanachama wa Young Africans kwamba tayari tumeshasaini mkataba, nitakuwa nawadanganya ila tunamuhitaji na tunamfatilia na tunaendelea kuwa na mazungumzo naye kama tutafikia mwafaka mzuri tutamleta klabuni kwetu.”