Imefahamika kuwa Msafara wa Klabu ya Simba utakaoelekea Niamey-Niger kwa ajili ya Mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Utakua na Wachezaji 24 akiwemo Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama.
Msafara wa Simba SC unatarajiwa kuondoka Dar es salaam-Tanzania kesho Ijumaa (Februari 18), tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa pili wa ‘Kundi D’ dhidi ya US Gendermarie, utakaopigwa Jumapili (Februari 20), Uwanja wa Général Seyni Kountché, saa moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Chama ataambatana na Kikosi cha Simba SC, kwa kazi maalum ya kiufundi, kufuatia kanuni za usajili za ‘CAF’ kumnyima nafasi ya kucheza mchezo huo, kutokana na kuitumikia RS Berkane ya Morocco kwenye michezo ya hatua za awali.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Mulamu Ngambi amesema tayari walishatuma wajumbe kwenda Niger kufanya uchunguzi na wamekamilisha taratibu zote za usafuri wa ndani, sehemu ya kufikia na chakula katika kipindi chote watakachokua mjini Niamey.
Baada ya mchezo dhidi ya US Gendermarie, Simba SC itaunganisha hadi nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko watatu wa ‘Kundi D’ dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Ikiwa nchini Morocco, Chama anatarajiwa kuwa sehemu ya msaada mkubwa kwa Benchi la Ufundi na Wachezaji wenzake, ili kufanikisha mpango wa kuikabili RS Berkane, ambayo aliwahi kuitumikia kabla ya kuamua kurudi Simba SC wakati wa Dirisha Dogo mwezi Januari 2022.
Katika Msimamo wa ‘Kundi D’ Simba SC ina alama 3 sawa na RS Berkane ya Morocco, huku ASEC Mimosas (Ivory Coast) na US Gendermarie (Niger) zikiwa katika nafasi mbili za mwisho.