Mlinda mlango wa klabu ya Real Sociedad ya nchini Hispania Geronimo Rulli, anatajwa kuwa kwenye mipango ya kusajiliwa na Pep Guardiola katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Gazeti la The Daily Mail limeandika kuwa, Guardiola amepanga kufanya usajili wa mlinda mlango huyo kwa lengo la kutaka kumpa changamoto Claudio Bravo ambaye ni chaguo lake la kwanza.

Gazeti hilo limeendelea kubainisha kuwa, mlinda mlango chaguo la pili klabuni hapo Willy Caballero ameshindwa kumshawishi meneja huyo kutoka nchini Hispania kumtumia kama sehemu ya kutatua tatizo hilo.

Caballero anatarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu, mkataba wake utakapofikia kikomo.

Tayari imefahamika Man City imetenga kiasi cha Pauni milioni 13.2 kwa ajili ya usajili wa Rulli.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 24 aliwahi kusajiliwa na Man City mwishoni mwa msimu wa 2014-15, lakini mwanzoni mwa msimu huu aliuzwa kwa Pauni milioni 4 katika klabu ya Real Sociedad.

Kabla ya kusajiliwa moja kwa moja na klabu ya Real Sociedad, mlinda mlango huyo alipelekwa kwa mkopo.

Video: Mpinga apiga marufuku taa za mwanga mkali kwenye Magari
Nape aahidi ushirikiano na vyombo vya habari