Meneja wa klabu bingwa nchini England (Leicester City) Claudio Ranieri amekubali kubeba mzigo wa lawama, baada ya kikosi chake kukubali kubanjuliwa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Southampton hapo jana.
Leicester City walikubali kipondo hicho wakiwa ugenini St Marries na kuendelea kusalia katika nafasi 15 kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka nchini England.
Ranieri aliwaambia waandishi wa habari kuwa, sio vyema kwa mchezaji wake yoyote aliyecheza katika mchezo huo kulaumiwa kwa kupoteza mbele ya Southampton, na badala yake akaomba lawama kuelekezwa kwake.
Alisema anajua nini alikifanya kwa lengo la kushindana kwenye mchezo huo, lakini mambo yalikwenda tofauti na kujikuta wakipoteza.
Mabao ya Southampton katika mchezo huo, yalifungwa na James Ward-Prowse, Jay Rodriguez pamoja na Dusan Tadic.
Leicester City aliotarajiwa kutoa upinzani mkali kufuatia juhudi walizozionyesha msimu uliopita hadi kutwaa ubingwa wa PL, wanamiliki point 21, ikiwa ni tofauti ya point 5 dhidi ya Sunderland wanaoburuza mkia.
Wakati huo huo mabao yaliyofungwa na beki kutoka nchini Ujerumani Shkodran Mustafi na mshambuliaji wa Chile, Alexis Sanchez yalitosha kuipa ushindi Arsenal dhidi ya Burnley waliopata bao moja.
Bao la Burnley lilifingwa na Andre Gray.