Kaimu Mwenyekti wa klabu ya Young Afrcans Clement Sanga mchana huu ametangaza kujiuzulu, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kongwe nchini.
Sanga amejiuzulu nafasi hiyo kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri baina yake na viongozi wenzake ndani ya klabu hiyo ikiwemo wale wa Kamati ya Utendaji kueleza kuwa hana ushirikiano mzuri.
Kiongozi huyo aliyekuwa akikaumu nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Young Africans, Yusuf Manji, alikuwa akitupiwa lawama na viongozi wa Kamati ya Utendaji akiwemo Khalfan Hamis ambaye amejiuzulu juzi akidai Sanga amekuwa si mweledi wa mambo.
Pia kiongozi huyo alikua anashutumiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wanachama kwa kutajwa kuwa chanzo cha mwenendo mbaya wa kikosi cha Young Africans ambacho hakifanyi vizuri kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika CAF hatua ya makundi.
Mbali na matokeo mabaya ya michuano hiyo ya Afria, pia wanachama waliwahi kumshutumu Sanga kuwa sababu za klabu yao kupoteza ubingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2017/18, uliochukuliwa na watani zao wa jadi Wekundu Wa MSimbazi Simba.
Sanga amechukua maamuzi ya kujiuzulu nafasi yake klabuni hapo, kwa kutoa sababu za kusambaa kwa clip ya video mitandaoni zinazohamasisha wanachama kufika nyumbani kwake na kumshambulia kwa mapanga endapo angeendelea kubaki madarakani.
Sanga amesema naamini ni wakati mzuri kutangaza kujiuzulu nafasi yake, japo anatambua kuna baadhi ya wanachama wa Young Africans wataumizwa na maamuzi aliyoyachuku hii leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es salaam.
Ukiachana na Sanga, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa naye amethibitisha rasmi kuachia ngazi leo kutokana na kusumbuliwa na masuala ya kiafya.