Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Ziwa na Wakurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi – CMA, wameanza kikao kazi kilichoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi – WCF, ili kuwajengea uelewa wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Kifungu cha 5, Sura 263 marejeo ya mwaka 2015.
Kikao hicho kilichofunguliwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma jijini Mwanza, kilifuatiwa na kikao kama hicho kilichofanyika Juni 9, 2023 mjini Bagamoyo na kuhudhuriwa na Majaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, kutoka Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, pamoja na wakurugenzi wa CMA.
Akizungumza na washiriki hao, Dkt. Mduma amesema, Mahakama ni chombo muhimu katika mchakato wa ulipaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi walizoajiriwa kwa mujibu wa mkataba nsa kwamba mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuzitaka taasisi za umma kuongeza ufanisi na ubora wa utoaji huduma kwa wananchi.
“Kwa hivyo Mahakama na CMA ni wadau muhimu katika utekelezaji wa sheria ya fidia kwa wafanyakazi lakini pia tunajenga uelewa wa pamoja, kikao kazi hiki, kitaleta manufaa makubwa ikiwemo kuimarisha mahusiano, kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia kwenye kukuza uchumi wa nchi yetu.” Alifafanua Dkt. Mduma.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Joseph Mlyambina ameipongeza Menejimenti ya WCF kwa kuwa tayari kushirikiana na Mahakama pamoja na taasisi zinazohusu utatuzi wa migogoro ya kazi katika eneo la kujenha uelewa wa sheria ya fidia kwa wafanyakazi.