Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikisimama kupisha michuano ya timu za Taifa, Kocha wa Wagosi wa Kaya Coastal Union, Mwinyi Zahera ameifungia kazi safu ya ushambuliaji ambayo imeshindwa kupachika mabao mpaka sasa.
Wagosi wa Kaya wenye maskani yao mkoani Tanga wanaburuza mkia kwa kuambilia pointi mbili pekee kwenye michezo mitano mpaka sasa.
Katika michezo hiyo Coastal Union imeruhusu mabao saba huku ikitikisa nyavu mara mbili pekee na kumfanya Mcongo huyo kukuna kichwa kwa timu yake kubaki mkiani.
Amesema katika muda huu anaifanyia kazi safu hiyo ambayo imeonekana kutomkosha japokuwa muda wa kujirekebisha upo na anaimani na wachezaji wote kikosini.
“Ninao wachezaji wazuri akina Ibrahim Ajib lakini nashangaa kwa nini hawafungi, hivyo wakati huu ligi haichezwi nafanyia kazi suala hilo,” amesema Zahera.
Naye Katibu wa Wagosi wa Kaya, Omary Ayoub amesema hata viongozi wameona upungufu katika nafasi hiyo lakini wanaamini Zahera atawavusha na kuwafikisha katika malengo waliyoyapanga msimu huu.
Amesema ushindani umekuwa mkali kwa kila timu hivyo kusababisha wachezaji kukamiana zaidi katika michezo.
“Ligi Kuu sio mchezo, kwani kuna timu zina kila kitu na zinapambana kweli kweli kupata matokeo mazuri ni sehemu tu ya mchezo, naamini tutakaa sawa na kufanya vizuri mwanzo ni mgumu na ushindani ni mkali mno,” amesema Ayoub.