Wagosi wa Kaya Coastal Union wametamba kuanza vyema msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021-22, kwa kuifunga Azam FC kwenye mchezo wa ufunguzi utakaopigwa leo Jumatatu (Septamba 27) Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Coastal Union ambayo ilinusurika kushuka daraja msimu uliopita imetamba kufanya vizuri mbele ya Azam FC kupitia kwa Kocha wao Melis Medo, ambapo amesema amekiandaa vizuri kikosi chake na hana shaka na harakati za kusaka alama tatu muhimu.
Medo amesema anawaheshimu Azam FC ni timu nzuri na wao pia wako vizuri na tayari kwa ajili ya kutafuta matokeo mazuri kwa mchezo huo kupata pointi muhimu.
“Tuko tayari kukabiliana na Azam FC, kila kitu kinaenda vizuri na wachezaji wangu wako fiti kupambana na kuendelea kutumia vema uwanja wetu wa nyumbani,” amesema Medo.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya kwenda kupata matokeo ugenini dhidi ya Coastal Union.
Amesema baada ya kumaliza mechi ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, wachezaji walipewa mapumziko mafupi na wamerejea kwa ajili ya kuendelea na mapambano ya msimu mpya wa ligi hiyo.
“Ligi itakuwa ngumu, timu nyingi zimejiandaa kuanzia usajili hata maboresho ya benchi la ufundi, tuko vizuri kwenye maandalizi yetu msimu huu kutafuta matokeo mazuri kwa kila mechi iwe ugenini ama nyumbani,” amesema kocha huyo.
Kwa misimu mitatu, Azam FC hawajawahi kupata ushindi katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, baada ya msimu wa 2018/19, Februari 19 kuambulia sare ya bao bao 1-1, kisha Desemba 29 msimu wa 2019/20 kuchapwa bao 1-0 na msimu uliopita Februari 11, mwaka huu kulambwa mabao 2-1.