Klabu ya Coastal Union imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Biashara United katika mchezo wa pili wa ligi kuu Tanzania.
Mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Mkwakwani mkoani humo umeshuhudia timu hiyo iliyorejea ligi kuu msimu huu ikicheza kandanda safi katika vipindi vyote viwili na hatimaye kuwapa wakazi wa mkoa huo furaha ambayo waliikosa takribani misimu miwili mfululizo.
Bao pekee la Coastal Union lilifungwa katika dakika ya 20 ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Simba, Haji Ugando akiunganisha krosi safi katika kasi ambayo ilimshinda mlinda mlango wa Biashara United, Balora Nasridine.
Aidha, kwa ushindi huo, sasa Coastal Union inafikisha alama 4 baada ya kutoka sare na Lipuli Fc katika mchezo wa kwanza wa ligi uliofanyika katika uwanja huo wa Mkwakwani Jumanne ya wiki hii.
Kwa upande wa Biashara United ambayo pia imepanda ligi kuu msimu huu, inabaki na alama 3 ambazo ilizipata katika mchezo wa kwanza ilipoifunga Singida United katika uwanja wake wa nyumbani wa Namfua.
Wagosi wa Kaya, Coastal Union iliporomoka daraja pamoja na timu ya Mgambo JKT ya mkoani humo msimu wa 2015/16 hali iliyopelekea wakazi wa mkoa huo kukosa burudani kubwa ya soka hasa ligi kuu bara kwa muda mrefu, wazi kuwa urejeo wa timu hiyo pamoja na matokeo inayoyapata ni furaha kubwa kwao.