Imeelezwa kuwa wafungwa 23 wamefariki dunia na wengine 83 wamejeruhiwa katika kile ambacho mamlaka zinadai kuwa ni vurugu za kujaribu kutoroka gerezani kutokana na sintofahamu iliyopo juu ya mlipuko wa virusi vya Corona.
Waziri wa Sheria wa Colombia, Margarita Cabello amekanusha uwepo wa mazingira hatarishi ambayo yanaweza kuchochea maambukizi na Corona na kusema hakuna mfungwa au mfanyakazi yeyote wa magereza mwenye COVID-19 hivyo hakukuwa na sababu ya kufanya vurugu hizo.
Amesema hakuna aliyefanikiwa kutoroka na baadhi ya wafungwa waliohusika watafunguliwa mashtaka ya uharibifu wa mali na kujaribu kufanya mauaji.
Kumekuwa na vurugu katika magereza mbalimbali nchini humo ambapo wafungwa wamelalamikia idadi kubwa ya watu gerezani na huduma mbovu za afya ambazo ni hatarishi kwa kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona.
Colombia imeripoti maambukizi takriban 231 ya Virusi vya Corona na watu wawili wamefariki dunia mpaka sasa.