Mtahiniwa aliyeongoza kitaifa kwenye matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2021, Consolata Lubuva amesema Jitihada na juhudi katika masomo ndivyo vilivyomfikisha kuongoza taifa kati ya wanafunzi 422,388 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka 2021.
Akizungumza Jumamosi Januari 15, 2022 nyumbani kwao Salasala Jijini Dar es Salaam, Consolata amesema hakutarajia kuongoza kitaifa kwenye matokeo hayo bali ni kwa uwezo wa Mungu.
Consolata ameeleza kwamba siri ya mafanikio yake ni kumuomba Mungu, ushirikiano kutoka kwa walimu, wazazi na wanafunzi wenzake pamoja na jitihada zake binafsi.
“Nitakwenda kusoma PCB ili niwe daktari niweze kuwasaidia watoto wadogo, napenda sana kuwasaidia watoto wadogo ili wakue vizuri, na nitaongeza juhudi zaidi ili nifikie ndoto ya kuwa daktari wa watoto.” amesema mhitimu huyo aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa.
Aidha, Consolata amefaulu kwa kupata daraja A akiwa amefaulu masomo yote 10 yakiwemo ya sayansi na hisabati kwa kupata alama A kila somo.
Mama mzazi wa Consolata, Beatrice Halii alisema amefurahi binti yake kufaulu vizuri mtihani huo na kusema alitarajia
matokeo hayo kwa sababu ya juhudi ya masomo na maombi ya mtoto wake.
“Kwa kweli familia tumefurahi sana, nilitarajia matokeo mazuri kwake, Conso ni binti mwenye juhudi ya masomo lakini pia anamcha Mungu, anapenda kusali na kwenda ibada, hata wakati wa likizo zake ratiba yake tu ilinionesha atafanya vizuri mitihani yake na kweli kafanya, tunamshukuru Mungu,”alisema mama mzazi wa Consolata.
Aliongeza kuwa matokeo hayo ni mwendelezo wa juhudi zake za masomo kwani hata akiwa shule ya msingi alifanya
vizuri na alisoma shule moja ya masista na ndio walioishauri familia hiyo baada ya matokeo kuwa aende St Francis kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Tulifuata ushauri wa shule aliyosoma msingi, sista aliyekuwa nae wakati akisoma shuleni hapo msingi, ndiye aliyejua mwenendo wa Conso na alitushauri hata baada ya matokeo kutoka kwamba tumpeleke St Francis na wakati huo sisi tulishakuwa tumelipia shule nyingine, ila akasema yeye atatafuta shule na kweli ndio akasema Conso amepata nafasi St Francis aende,”alisema mama yake Consolata.
Beatrice aliongeza kuwa uwezo wa akili wa Consolata pia umechangiwa na asili yao kwani hata yeye na baba yake Conso wote wana elimu za juu ambapo mama ana Shahada ya Uzamivu (PhD) na mumewe yaani baba yake Consolata ana Shahada ya Uzamili.
“Namwambia tu mwanangu bado ana safari ndefu shuleni ndio kwanza ameanza, hivyo ajitahidi asome zaidi yetu sisi wazazi wake,”alisema
Msichana hiyo amewashauri wanafunzi ambao hawajafanya vizuri kutokata tamaa bali waongeze juhudi zaidi kwenye masomo yao na kumwomba Mungu awasaidie.
Matokeo hayo yalitangazwa Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde ambaye alisema jumla ya watahiniwa 422,388 sawa na asilimia 87.30 ya watahiniwa 483,830 wenye matokeo ya kidato cha nne wamefaulu. Mwanafunzi huyo ni miongoni mwa wanafunzi wa Shule ya Wasichana St Francis ya Mbeya ambayo imefaulisha wanafunzi wake wote 92 kwa kupata daraja la kwanza na kuongoza kitaifa kuwa shule bora kati ya shule 10 bora.