Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amekabidhi Tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ kwa Baraza la Wanawake Wafugaji – PWC, Tanzania baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kati ya washindani 500 kutoka nchi mbalimbali dunia.
Tuzo hiyo, imetolewa na Taasisi ya Global Centre on Adaptation – GCA, jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu ambako unafanyika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), ambapo Kiongozi wa Baraza hilo kutoka jamii ya Kimasai, Maanda Ngoitiko ndiye aliyeipokea kwa niaba ya Baraza hilo.
“PWC wameiheshimisha sana Tanzania na kuifanya isikike duniani na nina uhakika kabisa tuzo hii imetokana na juhudi binafsi za dada yangu Maanda za kuimarisha uwezo wa uongozi wa wanawake wafugaji kwa kuwajengea uwezo kiasi cha kufikia usawa katika kutoa maamuzi katika jamii zao,” amesema Waziri Jafo.
Akishukuru kwa tuzo hiyo Bi. Maanda amesema kuwa Baraza hilo linawahudumia wanawake na wasichana kutoka jamii za Wamasai, Sonjo, Akie na Barabaig na kusema PWC ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi kaskazini mwa Tanzania kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo ya jamii kupitia uwezeshaji wa wanawake na wasichana wa Kimasai.
Tanzania, inaendelea kushiriki katika Mkutano wa COP 28 sanjari na mikutano ya pembezoni (side events), mikutano ya uwili (bilateral meetings) na warsha ambapo watu zaidi ya 81,000 kutoka nchi zaidi 190 wanahudhuria.