Kiungo wa Ufaransa Blaise Matuidi amekua mchezaji wa pili wa klabu ya Juventus kuathiriwa na virusi vya Corona.
Mwanzoni mwa juma hili klabu hiyo ilithibitisha kesi ya kwanza ya ugonjwa wa Corona, iliyomkabili beki Daniele Rugani, ambaye tayari ameshatengwa.
Taarifa zinaeleza kuwa, kabla ya Matuidi kuthibitika ameathirika, tayari alikua amejitolea kujitenga tangu Machi 11, baada ya kuanza kuona dalili za ugonjwa huo.
Matuidi mwenye umri wa miaka 32, kwa msimu huu amecheza michezo 31 ya michezo yote, na kwa mara ya mwisho alionekana akiwa dimbani wakati wa mpambano wa ligi ya Italia dhidi ya inter Milan uliomalizika kwa Juventus kupata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.
Mchezo huo uliochezwa bila mashabiki, kufuatia hofu maambukizi ya virusi Corona iliyotanda, katika viunga vya miji ya Italia.
Tayari waziri wa michezo wa Italia Giuseppe Conte, ametangaza kusitisha shughuli zote za kimichezo nchini humo hadi Aprili 3, kufuatia maambukizi ya virusi vya Corona kuendelea kushuka kasi duniani.