Rais wa Marekani, Donald Trump amelazimika kufanyiwa vipimo vya virusi vya corona baada ya kuwepo taarifa kuwa amekutana na watu kadhaa ambao baadaye walionekana kuwa na maambukizi.
Taarifa ya ‘White House’ kwa umma iliyotolewa muda mfupi uliopita, imeeleza kuwa vipimo vimeonesha Rais Trump yuko salama.
“Wiki moja baada ya kupata chakula na afisa mwandamizi wa Serikali ya Brazil [ambaye baadaye alibainika kuwa na virusi vya Covid-19], leo Rais Trump amefanyiwa vipimo vya kina na amebainika kuwa hana dalili za kuwa na virusi vya corona,” amesema Mratibu wa vyombo vya habari wa Ikulu, Stephanie Grisham.
“Nimeendelea kufanya mawasiliano ya karibu na kikosi kazi maalum cha Ikulu, na tunahamasisha utendaji kazi wao kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kusambaa kwa virusi hivyo,” aliongeza.
Taarifa hiyo imekuja saa chache baada ya Ikulu hiyo kueleza kuwa Trump hatalazimika kupima virusi vya corona kwa kuwa hakuonesha dalili.
Hata hivyo, shinikizo la vyombo vya habari na mitandao ambayo ilitoa uthibitisho wa watu watatu waliokutana na Trump ambao baadaye walionekana wameathirika uliwalazimu wabadili uamuzi.
Naye Rais Trump ameeleza kuwa vipimo vitaendelea kuchunguzwa na majibu mengine yanaweza kutolewa baada ya siku mbili, lakini kwa sasa ameonekana hana dalili zozote za Covid-19. Alisisitiza, “niliamua kupima kwa sababu ya shinikizo la vyombo vya habari.”
Rais Trump alitangaza hali ya dharura na kutenga kiasi cha $50 bilioni kwa ajili ya kupambana na tishio la virusi vya corona nchini humo.