Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetangaza hali ya dharura na kuutenga mji wake mkuu (kuufunga), Kinshasa kama hatua za kupambana na kuenea kwa virusi vipya vya corona (Covid-19).
Rais Felix Tshisekedi alitangaza hatua hizo jana alipokuwa akilihutubia taifa hilo kupitia televisheni ya Taifa.
Alisema kuwa hatua hiyo itaambatana na kufunga mipaka yote ya nchi hiyo, kuzuia safari za magari, mitoni na safari za angani (ndege). Nchi hiyo pia imechukua hatua nyingi za kuzuia mikusanyiko na kudhibiti safari.
Hadi sasa nchi hiyo imeshatangaza visa 45 vya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na vifo vitatu.
Jumatatu, jiji la Lubumbashi ambalo ni la pili kwa ukubwa lilitangaza hali ya dharura na kuzuia watu kutoka majumbani kwao kwa saa 48 baada ya watu wawili kupatikana na virusi vya corona.
Watu hao wawili waliingia jijini humo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Congo wakitokea jijini Kinshasa, Jumapili mchana, kwa mujibu wa Gavana wa jimbo hilo, Jacques Kyabula. Gavana huyo alisema ndege hiho ilikuwa imebeba abiria 77.