Mapema asubuhi ya leo Machi 28,2020 jeshi la polisi nchini Kenya limewatia mbaroni mapadri wawili , ma sister na waumini 46 ambao walikuwa wanashiriki ibaada katika kanisa katoliki mjini Bungoma.
Imeelezwa kuwa wamekamatwa kufuatia kukiuka agizo la Serikali la kuzuia mikusanyiko ya watu zikiwepo ibaada ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Covid 19.
Kati ya waliokamatwa, watu 32 walikamatwa parokia ya kristo mfalme na 14 walikamatwa parokia ya mtakatifu paulo.
Kamanda wa polisi, kamishna msaidizi Michael Yator amesema watuhumiwa hao waliwekwa mahabusu kwamuda na baadae wakaruhusiwa kurejea nyumbani.
Wakati hayo yakijiri, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Hillary Mutyambai ameonya kuwa watu wote watakaokutwa nje kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi watawajibishwa kwa mujibu wa Sheria.
Onyo hilo linakuja siku chache baada ya Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta kutoa amri ya watu kutotoka nje katika muda huo ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya covid 19.
Hadi sasa Katika maambukizi 31 yaliyoripotiwa nchini humo, Nairobi ina Wagonjwa 21, ikifuatiwa na Kilifi (6), Mombasa (2), Kwale (1) na Kajiado (1).
Wagonjwa wawili kati ya 31 wana hali mbaya na wamelazwa Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU) katika Hospitali ya Aga Khan.
Waziri wa Afya nchini humo, Mutahi Kagwe amesema mmoja wao ni Mkenya na mwingine ni Raia wa Ufaransa.