Vyama kadhaa vya Soka Barani Ulaya vimelitaka Shirikisho la Soka Barani humo “UEFA” kuahirisha fainali zijazo za Michuano ya UEFA EURO 2020 hadi mwaka mmoja mbele ili Kutoa nafasi ya kukamilika kwa Ligi zao za ndani.
Ombi hilo kwa UEFA limekuja kufuatia hofu ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona ambao unaendelea kusambaa katika nchi mbalimbali duniani.
Tayari UEFA wamethibitisha kulipokea ombi hilo na kuanza kulifanyia kazi, na huenda wakati wowote wakalitolea majibu, ambayo yatatoa mustakabali wa kuahirishwa kwa fainali hizo ama kuendelea kama zilizopangwa.
Tayari shirikisho la soka nchini Italia limeshatangaza kusimamisha kwa muda michezo ya ligi za nchi hiyo kwa kuhofia maambukizi ya virusi vya Corona, huku ligi za nchi nyingine wakicheza bila mashabiki.
Fainali za mataifa ya Ulaya UEFA EURO 2020, zimepangwa kuanza Juni 12 hadi Julai 12, katika nchi kumi na mbili ambazo ni Azerbaijan, Denmark, England, Ujerumani, Hungary, Italia, Uholanzi, Jamuhuri ya Ireland, Romania, Urusi, Scotland na Hispania.