Bodi ya Ligi Tanzania (TPBL) imetangaza maazimio 4 baada ya Serikali kusimamisha shughuli za michezo nchini kwa kipindi cha siku 30 kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona.
Katika kikao kilichofanyika leo, Bodi imeazimia mambo manne ili kuhakikisha baada ya muda uliowekwa na Serikali kupita, ligi inaendelea katika mazingira salama.
Afisa Mtendaji wa Bodi Ligi (TPLB), Almas Kasongo amesema TPBL imetangaza kuunga mkono uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli zote za michezo kwa mwezi mmoja ili kudhibiti maambukizi ya visusi vya Corona na azimio la pili, wachezaji wote walamika kupimwa virusi vya Corona kabla ya kuendelea na mechi.
Azimio la tatu, michezo itachezwa bila ya mashabiki baada ya siku 30 za kusimamishwa kwa mashindano yote nchini katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Corona ulioingia nchini.
Aidha, Bodi imeazimia kuwa ligi imalizike ndani ya mwezi Juni ili kutoa nafasi kwa timu zitakazoiwakilisha nchi kimataifa kuendelea na mchakato wa mashindano ya CAF lakini pia bodi itaendelea kusimamia afya kipindi hiki cha tahadhari ya Corona.
Wakati huo huo Klabu ya JKT Tanzania Leo tarehe 18/03/2020 rasmi imevunja kambi yake kutokana na maelekezo yaliyotolewa Jana na Serikali kupitia Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa kuhusu zuio la kuwepo kwa mikusanyiko mbalimbali kutokana na kuwepo ugonjwa wa Corona hapa nchini.
Afisa habari wa JKT TanzaniaJamila Mutabazi amesema Leo uongozi umewaruhusu Wachezaji kwenda kwenye familia zao lakini umetakiwa kuendelea kujikinga na kufuata maelekezo yanayotolewa na serikali sambamba na wataalam wa afya.