Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka wamiliki wa ardhi wanaotaka kilipia kodi ya pango la ardhi kufanya hivyo kupitia mitandao ya simu za viganjani ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia maambukizi ya virusi vya Corona.
Dkt. Mabula mesema hayo wilayani Bariadi mkoani Simiyu wakati akizungumza na wakurugenzi na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu akiwa katika ziara ya kuangalia utendaji kazi wa sekta hiyo sambamba na kufautilia maagizo aliyoyatoa kuhusiaa na sekta ya ardhi.
Amesema, ni vizuri katika kipindi hiki ambacho kuna maambulizi ya virusi vya Corona wamiliki wa ardhi wakachukua tahadhari ya kutokwenda ofisi za ardhi kulipia kodi ya pango la ardhi na badala yake wafanye malipo kwa kutumia mitandao ya simu.
‘’Katika kipindi hiki ambacho kuna maambukizi ya virusi vya Corona wadaiwa pamoja na wale wanaotaka kilipia kodi ya pango la ardhi wakafanya hivyo kupitia mitandao ya simu pamoja na kutembelea tovuti ya wizara ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia maambukizi’’ amesema Dkt. Mabula
Aidha, Dkt. Mabula ameoneshwa kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji kodi ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu pamoja na mkoa huo kusifika katika masuala ya uwekezaji.
‘’Mkoa wa Simiyu mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi yako chini sana, lengo la makusanyo kwa mkoa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 ni kukusanya bilioni 10 lakini kiasi mlichokusanya hadi sasa ni milioni 190 tu sawa na asilimia 9.1, inaonesha hamjawa makini kufuatilia madeni’’ alisema Dkt Mabula