Idadi ya waliopoteza maisha kwa virusi vya corona nchini Marekani imefikia 20,637 katika kipindi cha saa 24 zilizopita na kuifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza duniani kwa idadi kubwa ya vifo vilivyosababishwa virusi hivyo.
Taarifa iliyochapishwa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins imeonesha idadi hiyo ya vifo nchini Marekani, ikiwa inazidi idadi ya vifo vifo 19,500 vilivyotokea nchini Italia.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Marekani imefikisha visa vya corona 534,494, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika nchi moja, ingawa bado kuna matumaini kwani watu 30,548 wamepona.
Jiji la New York limerekodi vifo vingi, ikiwa na vifo 7,844 vinavyotokana na virusi vya corona. Idadi hiyo ni karibu mara tatu ya vifo vilivyotokea Septemba 11, 2001 baada ya magaidi wa Al-Qaeda kufanya mashambulizi katika jiji hilo. Watu 2,753 walipoteza maisha kwenye shambulizi hilo.
Kwa ujumla, idadi ya maambukizi ya virusi vya corona duniani ni zaidi ya watu milioni 1.7, hadi kufikia leo, na zaidi ya watu 107,000 wamefariki dunia tangu viliporipotiwa Desemba 2019 nchini China.