Uongozi wa Mkoa wa Shinyanga umeunda timu ya wataalam wa afya kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kupambana na virusi vya corona, ikiwa ni pamoja na kutenga ‘karantini’.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Nuru Mpuya amesema kuwa tayari maeneo ya Karantini yameshatengwa ikiwa ni pamoja na Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga, Ushetu, Msalala, Tinde, Mwendakulima na Kishapu.
“Wataalam wetu pia wamepewa mafunzo na vifaa kwa ajili ya kumhudumia mgonjwa mwenye dalili za virusi vya corona. Tumetembelea maeneo mbalimbali na kuwapima wafanyakazi ikiwa ni pamoja na raia wa China kama sehemu ya hatua za awali,” alisema Dkt. Mpuya.
Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya virusi hivyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaosha mikono yao kwa maji safi na sabuni, kutosalimiana na watu wenye dalili za kuwa na Covid-19 na kuhakikisha wanafunika vinywa vyao wanapokohoa.
Jana, Rais Magufuli aliwataka Watanzania wote kuchukua tahadhari kwa nguvu zote dhidi ya ugonjwa huo, ingawa alieleza kuwa hakuna mgonjwa aliyepatikana nchini kwa upande wa Bara na Visiwani.
Alisitisha safari zote za nje kwa wafanyakazi wa umma akieleza kuwa watapewa kibali endapo kutakuwa na sababu muhimu sana.
Nchi kadhaa za Afrika zimethibitisha kupata mgonjwa wa virusi vya Corona. Ndani ya siku mbili, Kenya, Rwanda, Ethiopia na Sudan walithibitisha kuwepo kwa virusi hivyo nchini kwao.