Serikali kupitia wizara ya afya imetangaza idadi mpya ya waliopona virusi vya covid-19 nchini Tanzania leo Aprili 7, 2020 kuwa ni watu wawili, na kufanya idadi ya waliopona kuwa watano tokea virusi hivyo viingie nchini.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa miongoni mwa waliopona, mmoja alikuwa mgonjwa Dar es salaam na mmoja mgonjwa wa Arusha na hivyo kufanya Arusha kutokuwa na mgonjwa yeyote wa Corona.
“Habari njema, wagonjwa 2 wa COVID19 wamepona, Dar es Salaam 1 na Arusha 1. Hivyo sasa Mkoa wa Arusha hauna mtu mwenye maambukizi ya COVID19” amebanisha Waziri Mwalimu kwenye ukurasa wake wa Instagram mchana wa leo.
Kwamujibu wa taarifa za wizara ya afya, hadi sasa Tanzania vimethibitishwa visa 24, waliopona 5, kifo kimoja, walio karantini ya lazima 72, waliomaliza karantini 375, na wanaofuatiliwa ni 366.
Aidha ametoa wito kwa jamii kuendea kufuata maelekezo ya Wataalam wa afya ikiwemo kuepuka mikusanyiko au misongamano isiyo ya lazima.