Kilio cha ugumu wa maisha na kudorora kwa uchumi kutokana na hatua za kudhibiti maambukizi ya corona, kimekuwa kikubwa zaidi ya kilio cha madhara ya kiafya yanayotokana na maambukizi hayo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Infotrack nchini Kenya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, infotrack imebaini kuwa hivi sasa covid-19 inaonekana kwanza kama tatizo la kifedha kwa asilimia 41 kutoka ilivyokuwa asilimia 28 mwezi Aprili.
Imeelezwa kuwa kiwango cha watu wanaoitazama covid-19 kwa pamoja kama tatizo la kiafya na kifedha kimeshuka kutoka asilimia 63 hadi 35, na sasa Wakenya wanaoliona kama tatizo la kiafya moja kwa moja ni asilimia 16 tu.
Utafiti huo unaonesha kuwa mlipuko wa covid-19 unajionesha kwa Wakenya wengi kama tatizo la kiuchumi hadi sasa ikiwa ni zaidi ya miezi mitatu tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa nchini humo.
Alisimia 87 ya Wakenya walioshiriki utafiti huo wameonesha kuwa bei ya vyakula imepanda, asilimia 79 wanashindwa kutuma fedha nyumbani kwao (vijijini) wakati asilimia 75 wameshindwa kulipa mikopo yao.
Aidha, imeonesha kuwa asilimia 68 wameshindwa kumudu ipasavyo kupata umeme, mafuta na mkaa, asilimia 67 wameshindwa kulipa bili za maji na umeme, asilimia 67 wameshindwa kununua dawa.
Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa asilimia 63 ya wakenya hawawezi kulipa kodi za nyumba kwa muda na asilimia 60 wameshindwa kulipa kikamilifu kodi ya nyumba (kukamilisha kiasi cha kodi).
Asilimia 54 ya waajiriwa wameripoti kuwa wamepunguziwa kiasi cha ujira wao, na asilimia 47 ya Wakenya wote hivi sasa wanategemea pia misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyakula vinavyotolewa na wasamaria wema.
Hali hii imebainika licha ya Serikali ya Kenya kufanya juhudi za kuwasaidia kiuchumi wananchi wake, ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha makato ya kodi. Serikali imepunguza kiwango cha makato ya kodi ya makazi na kodi katika biashara za kati na ndogo pamoja na kuondoa tozo mbalimbali.
Hadi sasa, Kenya imeripoti visa 4,738 vya corona, vifo 123 vitokanavyo na virusi hivyo. Hata hivyo, wagonjwa 1,607 wameripotiwa kupona.
Trump ataka upimaji corona upunguzwe kasi, adai upimaji unaongeza idadi ya visa
Rais Magufuli ataja sababu za kumuondoa Gambo na viongozi wengine Arusha