Nahodha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uingereza, Wayne Rooney amesema kuwa Serikali ya nchi hiyo imewachukulia wachezaji kama wanyama wa kufugwa katika hatua za kupambana na maambukizi ya virusi vipya vya corona.
Uingereza imeahirisha michezo yote ya soka hadi Aprili 3, 2020 itakapotoa tangazo lingine. Waratibu wa Ligi Kuu ya Uingereza wameeleza kuwa hali itabainisha yenyewe lini michezo itarejea katika hali ya kawaida.
Rooney ameandika ujumbe mrefu mtandaoni akieleza kuwa uongozi wa soka nchini humo umekosa ubinadamu, hawakuwafikiria wachezaji kuchukua hatua ya kuahirisha michezo haraka hadi pale baadhi ya wachezaji na makocha walipoonesha dalili za kuwa na virusi vya korona.
“Michezo mingine yote kama tennis, mbio za magari za Formula 1, rugby, golf na soka kwenye nchi nyingine ilikuwa imeshafungwa lakini sisi tuliambiwa tunapaswa kuendelea,” aliandika.
“Nadhani wachezaji wa mpira wa miguu walikuwa wanashangaa. Je, hii inatokana na pesa kuhusika kwenye mchezo huu? Kwanini tunasubiri hadi Ijumaa? Kwanini imesubiri hadi Mikel Arteta [Kocha wa Arsenal] kuugua ili Serikali ichukue hatua sahihi?
“Baada ya kufanya kikao cha dharura hatimaye uamuzi ulichukuliwa-hadi wakati huo tulihisi kama wachezaji wa mpira wa miguu Uingereza walikuwa wanatunzwa kama wanyama [aina ya guinea pigs]. Ninafahamu inavyojisikia. Kama mwanafamilia akiathirika kupitia kwangu kwa sababu nililazimika kucheza wakati ambapo sio salama, na wanaugua sana, ninaweza kufikiria sana kama ninaweza kucheza tena. Sitausamehe uongozi,” aliongeza.
Nchi mbalimbali zimechukua hatua ya kusitisha michezo, maeneo ya starehe, shule na maeneo ya kukutana pamoja kuabudu. Uingereza ni moja kati ya nchi za Ulaya zilizoathirika na virusi vya corona.