Bodi mpya ya shirika la hifadhi za taifa (Tanapa) imetakiwa kubuni mikakati ya kukuza utalii wa ndani na katika nchi za maziwa makuu na ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) baada ya tishio la kusambaa kwa virusi vya Corona kutoka kwa wasafiri, limeanza kuathiri sekta ya utalii nchini.
Ushauri huo umetolewa na Waziri wa maliasili na utalii Dk Hamis kingwangala wakati akizundua bodi mpya ya Tanapa makao makuu ya shirika hilo Jijini Arusha na kusema ni muhimu bodi mpya kuja na mbinu mbadala ili kuongeza mapato bila kutegemea watalii wa nje pekee.
”Sekta ya utalii inaweza kuathirika na mambo yaliyo nje ya mipaka ya Nchi yetu kama sasa kuna tishio la Corona, migogoro ya kidemokrasia na majanga mengine ya dunia ”alisema
Pia amesema kuna fursa ya kukuza utalii katika nchi za maziwa makuu na nchi za Sadc hivyo bodi mpya kwa kushirikiana na menejimenti ya Tanapa wanapaswa kutumia fursa hiyo.
”Mnapaswa kuongeza wawekezaji zaidi katika maeneo ya utalii na yale ambayo yanapendwa kama maeneo ya Serengeti na Ngorongoro kwa kuja na gharama za juu zaidi ili kuongeza mapato”amesema
Awali Kamishna Mkuu wa Tanapa DK Allan Kijazi alisema mlipuko wa homa ya Corona katika nchi za Asia tayari umeanza kuathiri ujio wa watalii nchini mwaka huu hali ambayo inatishia kushuka kwa mapato.
Kijazi amesema wakati mapato yakitarajiwa kushuka gharama za uendeshaji katika hifadhi zimeongezeka kutokana na miundombinu ya hifadhi kuharibiwa na mvua.
Amesema Tanapa imeanza kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli ya kuwa na kitengo cha ujenzi ndani ya Tanapa ili kushirikiana na majeshi mengine katika miradi ya ujenzi ambapo kitengo hicho kitazinduliwa machi mwaka huu.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Tanapa, Mkuu wa Majeshi Mstaafu Generali George Waitara amesema bodi yake itajitaidi kuhakikisha inatekeleza maagizo ya Rais John Magufuli na Wizara ya maliasili na utalii katika kuongeza mapato.