Klabu ya Tottenham Hotspur imethibitisha taarifa za mfanyakazi wake mmoja kubainika ameambukizwa virusi vya Corona.
Mfanyakazi huyo ni mtu pekee ambaye amethibitika kuwa na virusi hivyo katika kundi la watu 1,197 waliofanyiwa vipimo juma hili.
Hata hivyo klabu hiyo ya Kaskazini mwa London haijaweka hadharani jina la mfanyakazi huyo kutokana na sheria za kitabibu.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana, Tottenham ilisema kuwa tayari muhusika ameshaanza kuchukua hatua stahiki baada ya kubainika kuambukizwa virusi hivyo.
“Kwa sasa hana dalili zozote lakini atatakiwa kujitenga na kukaa mwenyewe kwa siku saba kuendana na protokali ya Ligi Kuu.
Tutaendelea kuchukua tahadhari na kufuata protokali ya kurejea mazoezini ambayo ni ya kuhakikisha uwanja wetu wa mazoezi unabakia kuwa salama na mazingira huru dhidi ya virusi vya Corona,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa kanuni za afya zilizopitishwa na serikali ya Uingereza katika kipindi hiki cha Corona, iwapo aliyeathirika angekuwa ni mchezaji, mechi za Tottenham zingelazimika kusogezwa mbele.
Ligi Kuu ya England inatarajiwa kurejea Juni 17 ambapo kutakuwa na mechi mbili. Mechi moja itakuwa ni baina ya Arsenal na Manchester City na nyingine itakuwa baina ya Aston Villa na Sheffield United.