Uwanja wa mazoezi wa klabu ya Aston Villa umefungwa kwa kuhofia maambukizi ya virusi vya Corona, ambayo yanaongezeka kwa kasi kubwa katika baadhi ya nchi za barani Ulaya.
Uongozi wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England umethibitisha kuufunga uwanja huo, baada ya asilimia kubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza na viongozi kukutwa na maambukizi ya Corona.
Mwanzoni mwa juma hili wachezaji wote na viongozi wa Aston Villa walichukuliwa vipimo, ikiwa ni utaratibu wa kawaida ambao unafanywa na vilabu vya soka nchini England na kwingine barani Ulaya.
Hata hivyo majadiliano bado yanaendelea baina ya madaktari wawakilishi wa vilabu kwa kushirikiana na chama cha soka nchini England (FA) na Premier League, ili kupata muafaka wa tatizo la maambukizi mapya ya Corona.
Kufuatia hatua hiyo kuna wasiwasi wa mchezo wa mzunguuko wa tatu wa kombe la FA kati ya Aston Villa dhidi ya Liverpool ambao umepangwa kuchezwa baadae leo Ijumaa, kuahirishwa.
Maamuzi ya kufunga uwanja wa mazoezi tayari yameshafanywa na vionvgozi wa klabu za Sheffield Wednesday na Middlesbrough.