Idadi ya watalii katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti imepungua kwa asilimi 99.6 kutokana na madhara ya mlipuko wa virusi vya Corona ambavyo vimesababisha kusitishwa kwa safari mbalimbali za watu ndani na nje ya nchi tofauti.
Mhifadhi mkuu wa hifadhi hiyo, Massana Mwishawa leo Machi 27, 2020 amesema idadi ya watalii imepungua kutoka wastani wa watalii 6000 kwa siku hadi 24.
Mwishawa amesema kuwa ugonjwa huo una athari kubwa kiuchumi hivyo kila mmoja analo jukumu la kuhakikisha kuwa anapambana na ugonjwa huo.
Amesema kutokana na hali hiyo hoteli nyingi za kitalii katika hifadhi hiyo zimesitisha huduma zake na kuwarejesha nyumbani watumishi wake kutokana na kutokuwepo wateja wa kuwahudumia.
“Hoteli kama Four season, Melia nakadhalika zimewarudisha majumbani wafanyakazi wao kwavile hakuna kazi za kufanya baada ya wateja kukosekana sababu kuu ikiwa ni huu ugonjwa hivyo kwa umoja wetu tushirikiane kuhakikisha kuwa tunaepuka” amesema Mwishawa.
Katika hatua nyingine amesema hifadhi ya Serengeti imechukua hatua katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kununua vipima joto viwili ambavyo vimewekwa katika geti za kuingia na kutoka katika hifadhi hiyo